Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF), imefuta adhabu dhidi ya wanafamilia wanne waliofungiwa
kushiriki masuala la soka kwa mwaka mmoja.
picha na mtandao
Wanafamilia hao ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa, James Mwakwinya;
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA), Blassy Kiondo;
Kaimu Katibu wake, Ayoub Nyaulingo pamoja na Ofisa Habari wa Simba, Haji
Manara.
Haji Manara alitiwa hatiani Aprili 23,
mwaka huu kwa makosa ya lugha chafu na za chuki kwa viongozi wa TFF na
kupotosha umma dhidi ya kadi njano ya mchezaji Mohammed Fakhi wa Kagera Sugar
ambako alifungiwa kushiriki masuala ya mpira kwa mwaka mmoja na faini ya Sh
milioni tisa.
Viongozi wa RUREFA walifungiwa kwa mwaka
mmoja na faini ya Sh. milioni mbili kwa kila mmoja kwa makosa ya kukiuka
maagizo ya viongozi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliyotaka wasitishe mchakato
wa uchaguzi mkoa kwa kuwa kulikuwa na rufaa iliyokatwa TFF.
Akizungumza na Wanahabari leo Julai 17,
2017 Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Tarimba Abbas, alisema viongozi
hao wamesamehewa adhabu zao kwa kuwa waliomba kupitiwa upya kwa mashauri yao na
kamati imeona ni bora kuwaachia huru ili kuendeleza masuala ya soka.
“Wapo wengi waliofungiwa wengine maisha
na wengine adhabu fupi, msamaha huu ni kwa wale ambao wameomba tu kupitiwa upya
kwa adhabu zao, pia milango ipo wazi kwa wengine ambao wanataka kupitiwa kwa
mashauri yao, lakini si kwa wale waliopanga matokeo uwanjani,” alisema Tarimba.
Kadhalika, Tarimba aliwaomba viongozi wa
TFF kuandaa semina ya Maofisa Habari na Viongozi wa Ligi Kuu na Ligi Daraja la
Kwanza (FDL) ili kuepuka maneno machafu ambayo yanasababisha wao kufungiwa.
“Inaonekana viongozi na Maofisa Habari
hawana maneno mazuri ya kuongea na wadau wa soka na ndio maana matatizo ya
kufungiwa yanajitokeza mara kwa mara, naamini wakipata semina hiyo itawasaidia
kujirekebisha na kupunguza kesi kama hizo,” alisema Tarimba.
Kwa niaba ya TFF, Ofisa Habari wa Shirikisho,
Alfred Lucas, wameyapokea mapendekezo hayo kutoka kwa Tarimba na kwamba
tutafanyia kazi ili kurekebisha makosa hayo kwa manufaa ya soka la Tanzania.
No comments:
Post a Comment